Baada
ya straika mpya wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo kuwapagawisha mashabiki
wa timu hiyo kwa uwezo wake mkubwa aliouonyesha juzi, sasa amegeukia
kwa Mrundi mwenzake, mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe akianza kwa
kutamba: “Hapana, Tambwe haniwezi niko vizuri zaidi yake.”
Mavugo
ambaye alikuwa akisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa klabu hiyo, kwa
mara ya kwanza juzi aliichezea timu hiyo dhidi ya AFC Leopards ya Kenya
katika mchezo maalum wa Simba Day na Simba kufanikiwa kushinda kwa mabao
4-0.
Katika
mabao hayo, Mavugo aliyeingia kipindi cha pili, alitoa pasi ya bao la
tatu lililofungwa na Shiza Kichuya kabla ya yeye mwenyewe kufunga hesabu
kwa kukandamiza bao la nne.
Baada
ya mchezo huo, Mavugo aliyetua Simba akitokea Vital’O alianza kwa
kuwatuliza mashabiki wa Simba kwa kusema kuwa huo ni mwanzo tu na kwamba
bado ana safari ndefu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi na kuipa
makombe timu hiyo.
“Nimefurahi
sana leo (juzi) kuona sapoti kubwa ya mashabiki na wachezaji wenzangu
na kufanikiwa kuibuka na ushindi, niseme kuwa huu ni mwanzo tu na kwamba
tutaendelea kufanya vizuri zaidi kwa kuwa nia yetu ni ubingwa wa msimu
ujao.
“Kuhusu
Tambwe, ninamfahamu, najua kwamba ni mfungaji bora wa sasa lakini
niseme tutapambana na nitamfunika. Ukiangalia katika ufungaji bora msimu
uliopita yeye ana mabao 21 lakini mimi nilifunga 30 kule Burundi.
“Ukirudi
katika msimu wa nyuma tena, yeye alifunga 14, mimi nikafunga mabao 32.
Sasa unaweza kuona hapo kwa haraka tofauti iliyopo, lakini kingine
naifahamu ligi ya Tanzania na ninaifuatilia, kwa hiyo najua ninaokwenda
kukutana nao,” alisema Mavugo.
Imeelezwa
kuwa vita ya Mavugo na Tambwe inatarajia kuwa kubwa zaidi utakapoanza
msimu mpya si kwa kuwa wanacheza katika timu mbili hasimu zaidi Tanzania
bali hata katika kuwania namba kwenye kikosi cha timu ya taifa ya
Burundi.
Katika
kikosi cha Burundi, kwa sasa Tambwe na straika aliyewahi kuichezea
Yanga na Azam, Didier Kavumbagu ndiyo mastraika tegemeo huku Mavugo
akiwa kama mbadala wa washambuliaji hao.
0 Comments
Post a Comment